NILIVYOFANYA INTERVIEW NA LUSIFA 13
Niliingia ndani kwangu lakini siku hiyo nilitaka niukomoe mzimu wa Jay Love, kwa kuufanyia sapraiz, nikaingia Google na kuitazama namba 9 ya Kiarabu ilivyo, kisha nikaichora pale chini kwa rangi nyekundu kama ufanyavyo wenyewe.
Lengo langu niukomoe au kuuonesha dharau mzimu wa Jay Love ili kama ukija ukute nimeshaandika unachotaka ukiandike. Nikalala nikitamani kama mzimu huo ukija usiku huo niweze kuuona utakachofanya baada ya kuona nilichokifanya.
Katikati ya usiku nikashtuka, nikaona mtu akiwa amevalia kanzu na kilemba, nikang’amua kuwa alikuwa ni Jay Love tena wakati huo akizidi kukosa afya ; “ Au kwa vile lile dude lililokuwa likininyonya na damu na kumpa uhai Jay Love lilikuwa limechomolewa kutoka mgongoni kwangu,” nilijiuliza na kuona huenda ni kweli.
Basi akawa anazungukazunguka kwa hasira, mkono wake wa kulia akiwa na kisu kikubwa huku mkono wa kushoto akiwa amemshika bundi, hapo ndiyo nikajua kumbe huwa anaandika pale chini kwa damu ya huyo kiumbe!
Mzimu huo ulioonekana kushindwa kufanya chochote ulitoa makelele ya kutisha sana, sikuogopa nikaamua kuamka na kusimama ili ujue kama siuogopi.
Nikakumbuka kuwa nilipaswa kutoonesha kuogopa ili usinidhuru, lakini nilipomsogelea niligundua alikuwa ameoza kabisa maana mwili wake ulikuwa unatoa wadudu, nilianza kuogopa. Haraka nikashtukia nikafikiria kitu kinachochekesha nikamfikiria Mzee Senga yule mchekeshaji wa Kaole, nikaanza kucheka.
Nikashangaa kuuona ule mzimu ukihema sana nikagundua kuwa kumbe ni kweli ukiudharau mzimu ukutishao huwa unakosa pozi kweli.
Basi nikaongeza kucheka na kufikiria mambo mengine mengi ya kuchekesha na kweli ukazidi kuishiwa nguvu hadi ukaanguka pale chini. Hatimaye mzimu wa Jay Love ulikuwa mikononi mwangu sasa..
No comments:
Post a Comment