NILIVYOFANYA INTERVIEW NA LUSIFA 01 “Lazima nilipiganie penzi langu kwa kumuokoa mke wangu Rabia kutoka mikononi mwa mzimu wa Jay Love. Wakati huohuo natakiwa kujiokoa mwenyewe kwenye ncha ya kifo nilichopangiwa na mzimu huo!” nilirudiarudia maneno hayo kama kwamba sikumuamini mama mkwe wangu. Nilijua haja ya moyo ilikuwa ni kuhakikisha mwenyewe kwa macho, japo kuwa vimbwanga nilivyoviona usiku wa kuamkia siku hiyo vilionesha wazi kabisa kuwa tayari nimeingia kwenye vita ya kishirikina. Nakumbuka ilikuwa imepita takribani miezi mitatu bila kuhudhuria ibada wala kumkumbuka Mungu, hivyo kwa kuwa nimeingia kwenye vita hii ya kiimani nilijiona nahitaji kuwa karibu na Mungu ili aniokoe. Nikaanza sasa kusali kabla ya kulala siku hiyo tena nikakumbuka Biblia yangu na kuanza kusoma baadhi ya mistari kwa imani kubwa, nikajimwagia na maji ya baraka, nikiamini nitafukuza nguyu zozote za giza zinazonisumbua hususani mzimu wa Jay Love. Hata hivyo nikiri kwamba kwa mara ya kwanza pia nilianza kuona nyumba yangu ikiwa kubwa mno tena inayotisha, hisia za mimi kufuatwa na mtu kila nikitembea nazo zilizidi. Tena nilizidi kujiona mzito kila saa zilivyozidi kwenda. Nililala usiku ule nikiwa nimechoka sana huku taa zote nikiziwasha maana ujasiri wa kulikabili giza ulinishinda. Mwishowe nilipitiwa na usingizi mzito lakini ghafla nilishtushwa na ukelele mkali kama vile mtu alinipigia mayowe sikioni mwangu. Nikashtuka huku jasho likinitoka kwa hofu, lakini nilishangaa kutoona mtu yoyote ndani kwangu, badala yake niliona kiza kikubwa kikiwa kimetanda chumbani kwangu huku ukimya ukiwa ni wa hali ya juu. Nilijivaa ujasiri huku nikisali sala kadhaa ninazozifahamu na kwenda kuwasha tochi ya simu yangu. Chakushangaza niliiona kitanda changu kikiwa kimezungukwa na maandishi ya Kiarabu yaliyoandikwa kwa rangi nyekundu ambayo nilikuja kuibaini ilikuwa ni damu.NILIVYOFANYA INTERVIEW NA LUSIFA 02 Asubuhi ilipojiri niliyapiga picha yale maandishi na kuyadeki, japo nilijisikia sipo sawa hata kidogo nikajikongoja hivyohivyo kuelekea kazini kwangu. Niliwahi na kufanya kazi zangu kwa kusuasua mno, kila mtu aliweza aligundua kwamba nina matatizo kwa kunitazama tu usoni. Kuna mwandishi mwenzangu niliyezoea kutaniana naye sana, anaitwa Omary, aliponiona alishtuka kama ameuona mzimu aliponiuliza kwa nini nipo vile, nikatamani kumwambia yanayonisibu lakini niliamua kumezea na kuzuga; “Najisikia homa kidogo, nimepanga kuelekea hospitali.” Ilipotimu usiku kama kawaida nilipitia kwenye mgahawa na kula kisha nikaelekea nyumbani kwangu. Kwa kuwa nilikuwa nimechoka sana nikaamua moja kwa moja kwenda kulala na nilipojiegesha nikapitiwa na usingizi moja kwa moja. Usiku wa manane, nilishtuka na kuhisi kuna mtu anatembea chumbani kwangu, nikasikia hatua moja baada ya nyingine, zile hatua zilifika hadi kwenye kitanda changu, na nikahisi kimeshika upande wa tendegu la kichwa changu. Nikasikia kitu kikiketi, nikashtukia nimeshikwa bega na kutikiswa kama vile naamshwa, nikavaa ujasiri nikainuka. Cha ajabu nilishanga kumuona msichana mzuri wa Kisomali akiwa ameketi kitandani kwangu tena akiwa hana nguo ya aina yoyote. Uso wake mlaini ulikuwa kama mwanga wa mbalamwezi, nywele zake ndefu zilitiririka hadi chini na kuziba matiti yake. Kifupi alikuwa amekamilika kila idara. Akanisogea kitandani kwangu na kunishika kifuani kwangu kwa mkono wake kama vile anataka nilale, nilipolala na yeye alifanya hivyohivyo akanikumbatia kama vile anataka nifanye naye mapenzi. Siyo siri nilishawishika kwa kiasi kikubwa kulala na yule binti lakini hali ya hatari ilinipitia nikamsukuma chini lakini nilishangaa akidondoka na kuyeyuka kama mvuke. Sikulala tena hadi asubuhi na nilipoamka nikashangaa kuona kitanda changu kikiwa na maandishi mengine, yakitofautiana kidogo na yale ya jana yake. Niliyapiga picha na kudeki nikijiuliza yalikuwa yana maana gani, ingawa tayariNILIVYOFANYA INTERVIEW NA LUSIFA 03 Mpaka muda huo nilikuwa tayari nimeshashuhudia vioja vya ushirikina kwa macho yangu mawili, lakini tofauti na watu wengine mimi kidogo nilikuwa jeuri mno, sikutaka kuziogopa nguvu za giza kiasi hicho kwa sababu kuna sehemu nilisomaga kuwa wachawi, majini na mizimu huja kwa njia za kutisha ili uogope na ukiogopa tu, ndiyo unawafungulia mlango kwenye ufahamu wako ili wakufanye wanachokitaka hususani kukudhuru. Hivyo njia pekee ya kuwakabili ilikuwa ni kuficha hofu yako kwa kuwatazama tu, ndiyo maana wengine huvuta bangi au kulewa sana ili kujikinga na mauzauaza hayo kwa kuwa uoga unapotea kabisa. Na hivi nilikuwa mpenzi wa kutazama muvi za kizombi ndo sikuwa ninaogopa kiviile. Lakini juu ya yote nilijua Jay Love kwa vyovyote alikuwa akinitumia ujumbe kupitia maandishi yale ya ajabu, hivyo basi nikalazimika siku hiyo kuamka na kumtafuta mtu wa kunitafsiria. Mtu pekee niliyekuwa nikimfahamu alikuwa ni Shehe mmoja, mtoto wa yule mnajimu maarufu Afrika Mashariki, wengi wanamkumbuka kuwa kwa kutabiri masuala ya vifo mfululizo vya Bongo Muvi enzi hizo na kweli vikatimia na hata mimi nilifahamiana naye baada ya kuripoti habari zake mara nyingi. Nilimpigia simu na alishangaa kusikia simuulizii masuala ya habari kama ilivyokuwa kawaida yangu. Alinikaribisha vizuri nyumbani kwake pale Magomeni Mwembechai. Bila kupoteza muda nikafika na kuingia moja kwa moja ofisini kwake, nilimsalimia na sikutaka kumueleza kiini cha matatizo yangu zaidi, moja kwa moja nilimtaka anielezee maana ya yale maneno ya Kiarabu niliyoyaona kwa kuwa nilifahamu hakuna mchungaji wala padre aliyekuwa akiyafahamu zaidi ya mashehe na huyo ndiye niliona anafaa zaidi na ni mwaminifu. Sikusema chochote nikafungua simu yangu na kumuonesha picha ya kwanza na ya pili ya yale maneno, kama kawaida yake akavaa miwani na kuzitazama kwa muda mrefu kidogo kisha akaguna. “Mh!”NILIVYOFANYA INTERVIEW NA LUSIFA 04 Sikuonesha kushtuka sana kwa mguno ule kwa kuwa sitaka kuonesha kutekwa sana na utaalamu wake kwa sababu japo kuwa nilimuamini katika kunitafsiria lakini sikumuamini katika siri za maisha yangu ndo maana sikumuelezea chochote zaidi ya kumtaka anipe maana ya maneno hayo ya Kiarabu. “Bwana Denis, hizi ni namba, hii ya kwanza inaitwa ‘ishrun’ maana yake ishirini. Na hii yenye maneno mengi inaitwa ‘tis’a ‘ashar’ maana yake kumi na tisa. Lakini jinsi zilivyoandikwa nahisi kuna jambo, vipi Denis upo kwenye tatizo gani?” Nikainua mabega kuonesha hakuna tatizo, nikamuaga na kuondoka zangu kwa sababu sikutaka nimwelezee matatizo yangu halafu aanze kuniambia mara oohoo! Umerogwa inabidi tusafishe nyota, mara ooh toa hela hii; halafu mwishowe niwe mvunja nazi wa kudumu. Sikutaka kufikia huko, ili mradi tatizo nilikuwa nikilifahamu, nikaazimia kupambana mwenyewe. Nikaunganisha matukio; la kwanza ni maneno ya mama mkwe kuwa mzimu wa Jay Love utaniua, la pili ni kitambaa kutoka kwenye vita niliyopigana ndotoni na Jay Love, la tatu ni hizi namba. Siku ya kwanza ilikuwa ishirini siku ya pili ni kumi na tisa, tena kwa maandishi ya damu niliumiza kichwa lakini sikupata jibu, giza liliingia nikalala bila kuwa na hamu hata ya kula. Nilishangaa kulala vizuri mno hadi asubuhi lakini nilipoamka kama kawaida nikashangaa kuona maandishi mengine yakiwa yamezunguka kitanda changu kama yale ya siku zote, nikaingia Google na kusachi namba za Kiarabu nikaziona zile nilizotafsiriwa na shehe, nilipoitazama namba ya siku hiyo ndiyo nikaona ikiwa na maana namba kumi na nane. Kwa maana hiyo ilikuwa wazi kuwa Jay Love ananihesabia siku kwa kuanzia ishirini na kurudi nyuma, nikajiuliza zikiisha nini kitanitokea? Itaendelea keshoNILIVYOFANYA INTERVIEW NA LUSIFA 05 Nilikaa kimya nikisikilizia, japo kuwa siku zilivyozidi kwenda ndiyo vituko vilivyozidi kushamiri huku afya yangu ikizidi kudorora kiasi cha kuomba ruhusa kazini. Siku moja nikiwa katika hali ya kukata tamaa nilinyanyua simu yangu na kumpigia mke wangu Rabia maana hakuwa akipokea siku zote nilizojaribu kumtafuta na sikuwahi kuongea naye tangu mara ya mwisho nilipompeleka hospitali, simu iliita, kwa mshangao alipokea mwanaume akaongea kwa lugha ya kiarabu, haraka nikagundua huyo ni Jay Love. Ilikuwa wazi sasa kuwa mzimu wake upo karibu na mke wangu Rabia. Kwa ubishi niliamua kwenda mitaa ya kwao ili angalau nimtie machoni mke wangu. Nilipita mtaani kwao nikiwa kama mfu mwili wangu ukiwa kama vile umetundikwa kwenye mifupa.Nikiwa na manguo mazito na kofia iliyonificha sura yangu nilikaa duka moja jirani na kwa kina Rabia nikawa naangalia ili mradi nimuone Rabia wangu. Nilikaa mpaka giza linaingia ndipo nilishangaa kumuona Rabia akishuka kutoka kwenye taksi ile ya yule dereva wa Ubungo; Devi, tena safari hii akiwa siyo peke yake bali akiwa na mwanaume aliyevalia nusu kanzu huku kichwani akiwa kiremba. Alionekana ni Jay Love na walionekana wanafuraha kweli. Sikuwa najua nilikuwa naota au ni kweli nilichokuwa nikikiona? Inawezekanaje Jay Love akawa na mwili tena wakati ni mzimu? Sasa kile kiburi cha kutotafuta mtaalamu wa kunitibia kikayeyuka kabisa nikafunga safari haraka kuelekea kwa yule Shehe.NILIVYOFANYA INTERVIEW NA LUSIFA 06 “Chochote kinachokusibu, ndani ya siku 10 lazima ufe!” alisema yule Shehe mara tu nilipoingia ofisini kwake na alionesha kuwa siriaz kweli. “Umeona nini kingine juu yangu; shehe,” nilimuuliza nikionesha siogopi kauli yake japo moyoni nilijua mkojo nusu unichuruzike. “Umebeba mzimu wa mtu aliyekufa na unanyonya sehemu ya maisha yako kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo wewe unavyozidi kufa huku wenyewe ukipata uzima,” yule shehe alizidi kupigilia msumari. “Shehe, umejuaje haya?”niliuliza. “Siku ya kwanza ulipokuja na kunionesha yale maandishi nilibaini yanahesabu siku zako za kuishi sababu ile rangi nyekundu hakika ilimaanisha kifo, hivyo sikukuacha urudi nyumbani peke yako nilikupa msaidizi; Jini… Denis unaamini katika majini?” aliniuliza. “Naamini yapo lakini yote kwa imani yangu tunayafahamu kama mapepo wabaya na tunayakemea,” nilimjibu akacheka kidogo na kuniambia maneno haya: “Mwanzo, Mungu aliumba viumbe vitatu. Wa kwanza aliumbwa kwa udongo; huyu ni mwanadamu, wa pili aliumbwa kwa mwangaza huyu ni malaika, wa tatu aliumbwa kwa moto usiona moshi huyu anaitwa jini. “Nafahamu uumbwaji wa jini haipo kwenye Biblia kwasababu Biblia kiasili imejumuishwa vitabu muhimu tu ambavyo vinaonesha mtiririko wa vizazi kabla na baada ya Masihi yaani Yesu Kristo. “Hapa na maanisha kuwa kuna vitabu vingi ambavyo vimeandikwa na manabii wengi wa zamani wa Kiisrael kama vile kitabu muhimu cha dini ya Wayahudi ambacho kinaitwa Talmud, kingine ni Kitabu cha Enoch babu yake Nabii Nuhu ambacho kinaelezea jinsi malaika walioasi walivyotupwa duniani na kuzaa majitu makubwa mpaka gharika kuu lilipotokea; hivi vyote viliachwa kwenye ujumuishaji wa Biblia hivyo kukosa asili ya uumbaji wa majini tofauti na Kuran. Nafahamu unakaribia kufa lakini lazima nikuelezee haya ili ufe ukiwa unajua nini utakifanya ukihamia ulimwengu wa pili.” Baada ya kusema hayo alisimama na kufungua kabati moja na kutoa kitabu kikubwa chenye michoro ya kutisha.NILIVYOFANYA INTERVIEW NA LUSIFA 07 Alifungua kitabu kile na kuketi akaniambia; “Hiki ni kitabu cha Majini kilichoandikwa na Mfalme Sueleman kwenye Biblia ni Mfalme Selemani mtoto wa Mfalme Daudi. Kinaitwa Lesser Key Of King Solomon. “Ndani yake kimebeba siri za majini na asili yao na jinsi mtu anavyoweza kuwamiliki, wakamtumikia kama walivyomtumikia Mfalme Sueleman mwenyewe, kwa sababu wao wana uwezo mkubwa wa kiutendaji kuliko mwanadamu, tulichowazidi wao ni kwamba sisi tumeumbwa kwa taswira ya Mungu, hivyo Mungu anatupenda sisi kuliko viumbe vyote alivyoviumba kwa maana hiyo vyote hivi vimeumbwa vitutumikie. “Utashangaa nikikwambia kuwa hata hapa tumezungukwa na majini wapatao 40 wote wakiwa katika himaya yangu, wanatusikiliza na kutuangalia, (nilijikuta nikigeuka na kutazama huku na huko lakini zaidi ya mimi na Shehe, chumba kilikuwa cheupe). Mwenyewe akasema “Denis huwezi kuwaona kwa macho ya kawaida mpaka ufungue jicho la tatu.” Baada ya kusema hivi nilianza kucheka kwa maana niliona uzushi, Shehe akakasirika. ghafla nikasikia kofi kubwa likitua usoni mwangu nisijue nani aliyenipiga, maana Shehe alikuwepo kitini pake. Kabla sijaongea neno nikashtukia nimenyanyuliwa juu hali nikiwa nimeketi hadi kichwa changu kikagusa juu ya dari, ila aliyeninyanyua sikumuona, nikiwa hukohuko juu Shehe akaniambia “umeamini sipo peke yangu?” Nikajibu kwa uwoga huku nikitikisa kichwa kuonesha nimekubali, akaongea maneno ya Kiarabu nisiyojua maana yake, kama vile anatoa amri kwa kiumbe nisichokijua, taratibu nikashushwa chini nikaketi kwa adabu saa hiyo.

at 12:57 AM

Bagikan ke

0 comments:

Copyright © Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top