Monday, December 18, 2017

KURUDI KWA MOZA: 35 Ikabidi Kulwa asukume kabati kwani hawakutaka kuandikia mate wakati wino upo, na kweli alivyosukuma kabati aliona mlango wa chumba kingine kinachoonekana kama choo cha ndani, Kulwa alitaka kuwa shahidi bado na kukisogelea kile chumba kisha akashika ule mlango ila aliganda pale pale, akawa anajaribu kuutoa mkono wake ila haikuwezekana na mara chumba kile kikaanza kutingishika na kuwafanya wengine yaani Sara na Doto waanguke chini huku Kulwa akiwa kaganda pale pale mlangoni na mara akaanza kukauka kama anapigwa na shoti ya umeme. Sara na Doto walitamani wakamsaidie ndugu yao lakini hawakuweza kwani chumba kilikuwa kinatingishika na wao wapo chini, ile hali ilizidi kuwa mbaya kwa upande wao na gafla ikakatika mara tu ya mlango wa kuingilia chumba kile ulipofunguliwa na aliyeingia alikuwa ni Salome, walibaki wakimtazama tu kasoro Kulwa kwani hata kilichoendelea hakujua na alikuwa amekauka kama kapigwa na shoti ya umeme, alionekana Salome akipuliza upepo kutoka mdomoni kwenda kwenye mkono ambao Kulwa alishika kitasa cha ule mlango mwingine, na gafla alijikuta kakiachia na kuanguka chini ila akiwa vile vile hajitambui, Salome akamwamuru Sara amkongoje Kulwa kutoka kwenye kile chumba kwani Doto alikuwa bado na maumivu ya kuungua. Kwahiyo Sara aliinuka na kuanza kumburuza Kulwa nje huku hofu ikiwa mmemtanda moyoni kuwa huenda Kulwa amekufa maana alikuwa kimya kabisa kama kabigwa shoti ya umeme na alikuwa amekauka kabisa, ila Salome alimwamuru Sara amvutie hadi nje kabisa ambapo Sara alimburuza Kulwa hadi nje kabisa, kwa hakika alichoka maana Kulwa alikuwa mzito sana, alimuhurumia kumburuza ila ilibidi afanye vile kwani hakuwa na jinsi zaidi ya kumburuza tu, ukizingatia alishapewa amri na Salome kuwa afanye hivyo kisha akarudi sebleni ambako Salome alikuwa amekaa na Doto, hapo Sara akauliza, “Hivi Kulwa atapona kweli?” “Angekuwa haponi wala nisingekusumbua kuwa umbebe. Na ulianzaje na wewe kuwapeleka wenzio kwenye kile chumba?” “Hata sijui kwakweli, ila nilitaka kuwaonyesha kuwa kuna chumba ambacho hatukifahamu humu ndani” “Haya sasa, faida yake umeiona? Kaka yako atapona ila itamchukua muda sana kurudi kwenye hali ya kawaida, familia mnazidi kuugua magonjwa yasiyoeleweka” “Sikuelewi” “Si huwa mnabisha nyie siku zote kuwa mama yenu ni mchawi! Haya sasa kama mama yenu si mchawi, kile chumba kwanini kipo kisiri? Na kwanini mtake kuumia sababu ya kukichunguza kile chumba?” “Unajua ni vigumu sana mtu kuamini kuwa mama yako mzazi ni mchawi” “Basi ndio hivyo, wakati nafanya kazi hapa kwenu. Siku niliyoamua kukichunguza kile chumba nilizimia muda mrefu sana” “Wakati unafanya kazi hapa kwetu!!!” Sara na Doto walijikuta wakishangaa kwani waliona Salome anaongea maajabu ukizingatia kwenye nyumba hiyo wamemjua badae sana ila yeye anawaambia wakati anafanya kazi pale kwao, ila Salome hawakuwajibu chochote ila aliwaambia wasitoke nje mpaka Kulwa atakapozinduka. Rose alikuja kushtuka na kugundua kuwa alilala pale usiku mzima na kazinduka kesho yake huku mwili wa mama jack ukiwa kwenye siti ya nyuma ya gari lake kama alivyouweka, alishangaa sana kisha kuanza tena kuendesha gari kwa haraka haraka hadi akafika nyumbani kwa mganga ila alimkuta akiwa amechukia sana, kwani aliposhuka tu kwenye gari lake na kukutana uso kwa uso na Yule mganga alishangaa akifokewa na Yule mganga, “Ndio umefanya nini sasa Rose?” “Sielewi” “Huelewi nini na umemtoa kafara rafiki yako? Nenda kamzike sasa” Rose alihisi kuishiwa nguvu kabisa kwani hakutegemea kama rafiki yake atakuwa amekufa, “Nisamehe mganga” “Na bora ungewahi jana ile ile, sasa mwili umeshapoa kabisa ndio unamleta kwangu? Nenda kazike tu” “Nisamehe tafadhari sijui cha kufanya” “Hujui nini? Nenda kazike” “Sijapanga kumtoa kafara rafiki yangu hata sijui imekuwaje” “Hivi wewe mwanamke una akili gani? Mwanzo si nilikutuma na dawa mtoni wewe nikakwambia ukimwaga utamuona mwanao kitandani halafu msukume mtoni, ila wewe ukamuona sijui Moza wako ukakimbia na hukuweza kumsukuma, sasa nimekupa dawa umwage mlangoni kwako, usiongee na mtu yeyote zaidi ukifika ndani uanze kutaja majina ya unaowatoa kafara. Ni kweli hujaongea chochote ila umeanza kumtaja rafiki yako huyu, ulikuwa na mpango gani nay eye zaidi ya kumtoa kafara tu. Na hiyo kafara haikusaidii chochote ni kama umetoa sadaka tu, haya nenda kazike mzoga wako” Rose alijikuta akikosa nguvu kabisa kwani haya mambo yalivyoenda ndivyo sivyo yalizidi kumchanganya akili na akaona kunapoelekea sasa hata yeye binafsi atajikuta amejiua kwa presha au kwa namna nyingine yoyote maana hakuelewa chochote, hakujua aanzie wapi kuzika au aishie wapi. “Sasa mimi nitamzikaje?” “Kwani hujui watu wanazikaje? Wewe mwanamke ni mjinga sana, rafiki yako kakusaidia kakuleta kwangu halafu umemtoa sadaka, yani wewe mwanamke ni mpumbavu” “Nakuomba mganga tumsaidie rafiki yangu kwa namna yoyote ile” “Tumsaidie nini na mwili umepoa huo? Labda utoe kafara ya watoto wako wote” Rose alichanganyikiwa kabisa, ila Yule mganga aliondoka na kwenda kwenye chumba chake cha uganga na kumuacha Rose akiwa na mawazo yasiyo na kifani. Aliwaza kuhusu watoto wake na kuona kuwa vyote alivyovifanya kwa kipindi chote ni kazi bure, “Hivi mimi si ndio nilimtesa yule mwanaume yani Patrick na kumfanya kama ndondocha sababu ya watoto wangu! Nilitaka waishi vizuri, wale raha ya maisha, yani leo nikawatoe wote kafara kweli! Hao wawili wenyewe nilikubali kwa shingo upande, naweza kuwatoa kafara watoto wangu kweli! Kuna sababu gani ya mimi kuendelea kuishi na kutafuta mali kwa haj azote ikiwa watoto angu nimewatoa kafara, kuna faida gani ya kuishi vizuri huku nikinyooshewa vidole na watu kuwa niliwatoa kafara watoto wangu! Nawapenda sana, niishi bila Sara, Kulwa, Doto na Ana kweli! Hapana kwakweli, na huu mwili wa rafiki yangu sijui nitafanya nao nini” Aliwaza sana bila ya jibu la mawazo yake na alijihisi ni mkosanji kila alipofikiria kwani aliona anapoelekea sasa sio kuzuri, yani awatoe watoto wake wote. Yule mganga akamtuma mtu ambaye alienda kumuita Rose na kuingia kwenye chumba cha mganga, na baada ya kuingia tu aliulizwa alichokiamua, “Utaenda kumzika rafiki yako au utawatoa watoto wako kafara?” “Nitaenda kumzika rafiki yangu” “Yani wewe naelewa sasa kwanini wachawi wenzio hawashirikiani na wewe, yani wewe uchawi wako mkubwa ni kutegemea nguvu za waganga wa kienyeji, hakuna mchawi ambaye hatoi kafara, wewe ni mchawi gani wewe? Nakuuliza mara ya mwisho, utaenda kumzika rafiki yako au utawatoa watoto wkao kafara?” “Nitaenda kumzika rafiki yangu” Mganga ilibidi acheke huku akisikitika, alimuangalia kwa makini sana Rose halafu akamwambia tena, “Nakupa machaguzi ya mwisho, nenda kafikirie kati ya kumzika rafiki yako na kuwatoa kafara watoto wako” Rose alitoka tena na kukaa chini ya mti huku kichwa chake kikiwa kimejawa na msongo wa mawazo. Kulwa alishtuka kama mtu aliyeshtuka usingizini halafu moja kwa moja akakimbilia ndani huku akihema sana, ni Sara aliyeenda kumdaka maana haikujulikana kuwa alitaka kukimbilia chumba gani ukizingatia Salome alishawaambia kuwa akili yake itakuwa kidogo inasumbua kufanya kazi kwa kipindi hiko kutokana na kuanguka kwenye kile chumba. Kwahiyo Sara alimshikilia kaka yake huku akimsihi kuwa akae kwanza akili itulie, ila Kulwa alipokaa tu alianza kuropoka kuwa kuna vitu aliviona wakati amelala, “Vitu gani hivyo?” “Kwanza mama yuko wapi?” “Hayupo, unajua fika mama tangu jana aliporudi na rafiki yake kuanguka akaondoka nae ndio hajarudi hadi leo” “Basi nilichokiona ni cha kweli” “Kitu gani hicho?” “Nimeona mama yupo kwa mganga, yani Yule rafiki wa mama wa jana eti amekufa” Wenzie wakashangaa na kuuliza, “Amekufa!!” “Ndio nilivyoona, na mama kapewa achague chaguo moja na Yule mganga, yani aende akamzike rafiki yake au atutoe sisi wanae kafara. Kwenye kumuona kwangu yani bado mama anafikiria kuhusu hilo swala kuwa atutoe kafara au akamzike rafiki yake” “Yani mama yetu atutoe kafara sisi!” Doto aliuliza kwa mshangao, na Kulwa akamjibu “Ndio, kapewa chaguo hizo kuwa atutoe kafara au akamzike rafiki yake” “Haiwezekani, haiwezekani mama kututoa kafara sisi. Hayo ni mawazo yako tu yasiyokuwa na maana yoyote Kulwa” Salome aliyekuwa akiwasikiliza tu akacheka sana kisha kumuangalia Doto na kumwambia, “Tena wewe ndio usiseme kabisa, nadhani leo ndio ingekuwa mazishi yako. Mama yako alishakubali muda mrefu sana kukutoa kafara wewe, na badae akakubali kukutoa wewe na Sara, ila kwa ninavyomjua angekutoa wewe kwanza” Wote walikaa kimya kwanza baada ya kusikia kuwa walikuwa kwenye orodha ya kutolewa kafara, na lile swala aliloongea Kulwa kuwa mama yao yupo kwenye machaguzi ya kuwatoa kafara wao au kumzika rafiki yake. Doto alijikuta akiuliza, “Jamani sasa tutafanyaje ikiwa mama atapanga kututoa kafara wote?” Kulwa akawaambia wenzie kwa msisitizo, “Jamani sikilizeni, kama mama alipanga kuwatoa kafara nyie mwanzoni ila Salome alipokuja na Yule mgeni wote tulimshangaa ila kumbe ndio ametolewa sadaka kwaajili yenu. Hapa hatuna budi zaidi ya kumwambia Salome atusaidie” Kisha akamgeukia Salome na kumwambia, “Salome tusaidie maana kwajinsi nilivyomuona mama anasuasua kwenye ndoto kwa hakika atachagua kututoa kafara tu, naomba utusaidie” Sara nae akachangia, “Kweli Salome tusaidie” Sasa nyie mnaniombaje hivyo binadamu mwenzenu badala mmuombe Mungu awasaidie, ombeni Mungu awasaidie na muelewe kuwa mama yenu sio mtu mzuri, kila siku nawaambia kuwa mama yenu sio mtu mzuri ila hamtaki kuelewa ila muelewe sasa, na mkitaka niwasaidie tushirikiane kwa pamoja ili mama yenu aachane na uchawi na arudi kwenye maisha wanayoishi binadamu wa kawaida” “Kwahiyo ni kweli mama kahifadhi watu kwenye kile chumba kidogo?” “Yani siku wakitoka mtashangaa sana, kwanza ni wamekonda mno halafu watu wengine hata hamuwezi kuwadhania kama wapo humo” “Mmmh hivi wewe Salome ni mtu wa kawaida kweli?” Salome akacheka na kuwaambia, “Mimi ni mtu wa kawaida ila ipo siku mtanijua mimi halisia kuwa ni nani na kwanini nilikuwa nafanya yote haya” Walijikuta wote wakitamani kumjua Salome halisia ni nani ila Salome aliwabadilishia mada na kuwataka kuwa wakapate chakula ila alimtaka Sara akamuite mlinzi ili siku hiyo ale chakula pamoja na mlinzi. Sara alifanya hivyo kwenda kumita mlinzi ila mlinzi aligoma na kusema kuwa hawezi kwenda kula ndani kwenye nyumba hiyo. “Kwanini?” “Sitakli tu, na siwezi kuja” Sara alirudi na kumpa huo ujumbe Salome ambaye alisema, sawa hakuna tatizo ila muda mfupi tu mlinzi alikuwa mezani akishangaa shangaa kuwa ameingiaje ndani ya nyumba wakati alikataa. Patrick na Neema muda huu waliamka tena na kujiona kuwa sasa wapo sawa kiasi yani ule uchovu umepungua pungua ila muda nao ulikuwa umeenda sana yani giza lilishaanza kutanda, waliamka na uchovu na kutoka sebleni ambapo Neema alianza kwa kumuita Salome ila ilikuwa kimya na kuhisi kuwa Salome hakuwepo, “Unajua huyu mtoto kipindi cha nyuma alisema kuwa anakuja kukaa nyumbani kwako ili akae karibu na baba yake, sasa kipindi hiki uko hapa ila mbona haonekani nyumbani?” “Labda kaenda kujisomea na wenzie” “Aende kujisomea wapi? Yule mtoto amekataa kwenda shule kama hujui, na ndio kwanza yupo kidato cha tatu ila kwenda shule amegoma sijui ataingiaje hiyo kidato cha nne mwakani maana miezi inazidi kukatika tu” “Kumbe hasomi? Kwanini umeacha mtoto hasomi?” “Sassa kakataa shule mwenyewe unadhani mimi ningefanyaje? Hivi unakumbuka kwanza mara ya mwisho kabla hatujarudi nyumbani tulikuwa wapi?” “Hata safari ya kurudi nyumbani sijui imefanyajwe fanyajwe. Ila Neema mchunguze mtoto, haiwezekani mtoto akatae tu gafla kwenda shuleni halafu wewe ukae unamchekelea tu, labda kaanza wanaume usikute wanamuongopea” “Mmmh kama nakumbuka kitu hivi, Salome aliniambiaga ana simu umemnunulia wewe” “Mmmh sijawahi kumnunulia Salome simu” Neema machale yakamcheza na kuanza kuhisi vile alivyoambiwa na Patrick kuwa usikute mwanae ana mwanaume ndiomana hataki shule, akaamua kwenda kupekua chumbani kwa Salome kuwa pengine anaweza kukuta hata barua ya mapenzi na ajuwe ni wapi aanzie na mtoto wake huyu. Wakati ameenda kupekua chumbani kwa salome, aliona begi dogo na kulifungua, alikuta simu ila alishtuka sana kwani ilikuwa ni simu ya Ashura. Rose aliitwa tena na mganga ili atoe chaguo lake alilolifikiria, “Muda unakwenda Rose, na usiku huo unaingia, chagua moja kumzika rafiki yako au kutoa kafara wanao” “Hapana kwakweli, kuwatoa kafara wanangu hapana, nipo tayari kumzika rafiki yangu” “Kumbuka utaenda kumzika peke yako na giza hili, hakuna wa kukusaidia. Chagua tena” Rose hakuwa na jibu la zaidi ya kumzika rafiki yake, “Kama umeamua hivyo sawa, inabidi azikwe leoleo yani maiti yake isilale tena maana yatatokea majanga bure” “Majanga gani?” “Usiniulize majanga gani, jua kuwa yatatokea majanga. Yani unatakiwa uizike maiti leoleo, ila kwa usalama wako ukiwa unatoka hapo mlangoni kwenda kuizika hiyo maiti usiongee na mtu yeyote Yule ila nenda moja kwa moja kuna mahali utakuta shimo halafu utamdumbukiza rafiki yako huku ukitaja majina yote ya watoto wako baada ya hapo utarudi na kulala hapa. Nadhani tumeelewana” “Ndio tumeelewana” “Haya lamba dawa hii na usiseme chochote” Rose akalamba ile dawa na kutoka nje, ila kabla hajalisogelea gari lake akashangaa kumuona mwanae Ana akiwa amemfata kule kwa mganga, alishangaa sana na kujikuta akisema, “Ana!” “Ndio ni mimi mama, nimekufata nata……” Ila kabla Ana hajamaliza sentensi yake, Rose alianguka chini na kuanza kutapatapa. Itaendelea kesho usiku…….!!!!!!!!!! By, Atuganile Mwakalile

No comments:

Post a Comment