MUME WANGU SHUJAA WANGU - 3 Baada ya kutulia, kwenye muda wa saa 3 asubuhi nilimpigia simu Anti Jessica lakini nikashindwa kuongea, badala yake nikawa nalia. Aliniambia kuwa angenifuata baada ya saa moja nami nikamwambia kuwa ni bora mimi nikimfuata badala ya yeye kuja. Njiani nilimpitia Hamasa ili anisindikize. Tulipofika nilimweleza Anti kila kitu kilichotokea na kunishauri kuwa nimpeleke Belinda kwenye shule ya bweni. Hata hivyo, tatizo ni kwamba alikuwa katika muhula wa pili wa masomo yake hivyo isingewezekana. Baada ya kutafakari kwa kina, Anti Jessica alishauri kuwa itakuwa vizuri yeye akiishi naye. Tulikubali wazo hilo na tulipofika nyumbani nikamwambia Belinda afungashe vitu vyake lakini alikataa na kuanza kuniuliza ni uhalifu gani aliofanywa wa kustahili kufukuzwa kama mbwa. Hamasa alikasirika na kumchapa kofi na kumwambia aache mchezo wa kujifanya kuwa hana makosa. Alilia, akasema kuwa hatokanyaga tena nyumbani kwangu na kuanza kunilaani kuwa laana ya baba yake itaniandama kwa kipindi chote cha maisha yangu. Sikuyaweka akilini yote aliyosema kwa sababu sikumfokea au kumpiga bali nilizungumza naye kwa uzuri tu… Nyumba yangu ilitengamaa na kila kitu kikarudi kwenye hali ya kawaida baada ya Belinda kuondoka. Katika muhula wa tatu kuelekea kwenye mitihani yake ya mwisho, alianza kuandika meseji kwenda kwa mume wangu kwamba aanze kumchukulia kuwa ni mkewe wa pili. Tukaenda nyumbani kwa Anti Jessica na kumwambia aache upuuzi wake aliokuwa akiufanya. Hata hivyo, tulishangazwa na ajibu lake kwamba hatoacha mpaka atakapopata anachokitaka. Nilihuzunika na kujiuliza kwa nini mtoto wa kaka yangu ambaye nilimsaidia na kumlea kama mwanangu afikie hatua ya kunifanyia hivyo? Baada ya Belinda kumaliza kidato cha nne alishika ujauzito wa mume wa mtu aliyekuwa akiishi jirani naye. Mwanaume huyo aliikataa mimba hiyo. Anti Jessica alimsaidia kumlea mwanaye Joshua nami pia nilikuwa nikimsaidia baadhi ya mahitaji. Joshua alipofikisha umri wa miezi 8, Belinda aliingia chuo na huko akabeba ujauzito wa mhadhiri mmoja mwenye mke… Mke wa mhadhiri huyo alimpa vitisho vikubwa, hivyo akalazimika kuitoa mimba yake. Utoaji wa mimba hiyo haukufanywa vizuri na katika mchakato huo, kizazi chake kiliondolewa. Nilijaribu kuongea naye lakini hakunisikiliza na kudai kuwa hakuna anayempenda, jambo ambalo sio kweli. Yuko mwaka wa mwisho wa masomo yake ya chuo na nina shauku kumuona akijitegemea ili aweze kujikimu. Anapokuwa na likizo huenda nyumbani kwa Anti Jessica. Bado anafukuzana na waume za watu na kila mtu humuita kuwa ni mvurugaji wa nyumba za watu. Wakati fulani watu hudai kuwa mama wa kambo au walezi ni wabaya lakini ukweli ni kwamba baadhi ya hao wanaolelewa wanakuwa wabaya sana. FUNZO LA SIMULIZI YANGU: 1. Wanaume wanatakiwa kujifunza namna ya kujidhibiti nyakati zote kwa sababu mitihani ipo kila mahala. Kosa moja linaloweza kuepukwa, linaweza kuiharibu nyumba yako maridhawa! 2. Mwanamke anayependa kuwashawishi waume za watu anatakiwa kuacha hiyo tabia, zamu yako itakuja. Je, utapenda mtu avuruge ndoa yako? Unapataje furaha baada ya kujua kuwa umevuruga ndoa ya mtu? Acha kuwapenda waume za watu kwa sababu hujui wametumia nguvu kiasi gani kuijenga ndoa ya. 3. Kama unalelewa, washukuru walezi wako na kama bado upo shule zingatia masomo yako kwa ajili ya kuwa na mustakbali wa maisha mazuri. Usiwe hasimu wa yule anayekupa hifadhi. 4. Kama mtu ameshachukuliwa amechukuliwa. Usijaribu kuharibu uhusiano wake eti kwa sababu unamtaka. # Ninathubutu kusema mume wangu ni shujaa wangu kwa sababu alivikabili vishawishi. Ninamshukuru sana kwa hilo na nitaendelea kumthamini daima dawamu. Hiyo ndiyo simulizi yangu… Ahsanteni sana wana- Ndoa Maridhawa. MWISHO

at 4:06 AM

Bagikan ke

0 comments:

Copyright © Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top